Folk Tale

Chura mwenye Majivuno

AuthorB.S. Mang'anda
Book TitleHadithi za Esopo
Publication Date1996
LanguageSwahili
OriginKenya

Alikuwepo Chura mmoja aliyeishi karibu na bwawa. Chura huyo aliishi na watoto wake wengi. Kila siku asubuhi Chura huyo aliondoka nyumbani kwake kwenda kutafuta chakula. Kila jioni aliporudi nyumbani aliwauliza wanawe habari za kutwa. Watoto walimweleza mama yao yote yaliyotokea. Baada ya habari, mama yao aliwapa chakula. Baada ya kula walilala.

Kila siku mambo yalikuwa hivyohivyo.

Siku moja Mama Chura alikwenda kutafuta chakula kama kawaida. Huku nyuma, ng'ombe alipita karibu na makazi ya Chura. Kwa bahati mbaya, akawakanyaga watoto wa Chura watatu wakafa.

Mama Chura aliporudi jioni aliwauliza wanae, "Habari za kutwa?"

"Mbaya mama," Watoto walijibu.

"Kwa nini?" Mama Chura akauliza.

"Hapa alipita mnyama mmoja mkubwa akakanyaga wenzetu watatu wakafa," Watoto walieleza.

Hapo Mama Chura akataka kujua ukubwa wa huyo mnyama aliyewakanyaga watoto wake. Hivyo, alijitunisha halafu akauliza, "Alikuwa kama hivi?"

Watoto wakamtazama mama yao na kumwambia, "Alikuwa mkubwa zaidi ya hapo."

Mama Chura alijitunisha zaidi na kuuliza tena, "Alikuwa hivi?"

Watoto walijibu, "Alikuwa mkubwa zaidi."

Mama Chura alijitunisha zaidi na kuuliza kwa shida, "Alikuwa hivi?"

Watoto wakamwambia, "Mama hata ukijitunisha vipi hutafikia ukubwa wa mnyama yule."

Mama Chura hakukubali. Alijaribu kujitunisha zaidi. Akapasuka na kufa.


Text view