Folk Tale

Fisi na Korongo

AuthorB.S. Mang'anda
Book TitleHadithi za Esopo
Publication Date1996
ATU76
LanguageSwahili
OriginKenya

Fisi anapenda sana kula mifupa na mizoga.

Siku moja, Fisi alipata mizoga mingi. Aliila yote. Kwa bahati mbaya, mfupa mmoja ulimkwama kwenye koo. Alijitahidi kwa kila njia kuutoa. Alikunywa maji ili maji yateremshe mfupa huo. Haukutoka. Aliwaomba wenzake wampige mgongoni kwa matumaini kwamba mfupa huo ungetoka. Haukutoka. Alikosa raha kabisa.

Akatokea Korongo akamwuliza, "Je nikikutoa huo mfupa utanipa zawadi?"

"Ndiyo," Fisi alikubali.

Hapo Korongo alimwambia Fisi aachame. Fisi aliufungua mdomo wake. Korongo akaingiza mdomo wake mrefu kinywani mwa Fisi. Akautoa ule mfupa.

Baada ya kutoa mfupa, Korongo alimkumbusha Fisi, "Vipi ahadi yako ya zawadi?"

Fisi alicheka sana halafu akauliza, "Zawadi ya nini?"

"Zawadi ya kukutoa mfupa," Korongo alijibu.

Fisi alitingisha kichwa na kusema, "Wewe una bahati. Shukuru sikufunga mdomo wangu na kumeza kichwa chako."


Text view